WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kufanya kazi zao kwa utaratibu na kufuata miiko na maadili ya taaluma yao na kutakiwa kutojiingiza katika mambo ambayo ni kinyume na taaluma ya uandishi wa habari.
Hayo yalisemwa jana na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Siasa (TAPOREA) na kufanyika jijini Dar es Salaam jana.
“Tasnia ya habari ina utaratibu wake na miiko yake na ninyi lazima mtii miiko hiyo…msijiingize katika mambo ambayo ni kinyume kabisa cha taaluma yenu,” alisema Sumaye. Sumaye alisema uhuru wa habari una pande mbili, hivyo mmoja usizuiwe kutafuta, kupokea na kusambaza habari na upande wa pili ni mwandishi kufanya kazi kwa kufuata utaalamu na miiko ya taaluma yenyewe.
Alisema mwandishi ukiandika habari za uongo bila kuzithibitisha ni makosa, lakini pia ni makosa kuandika kwa kumuandama mtu au kikundi kwa kumchafua kwa makusudi. Alisema mwandishi ukimwandika mtu vibaya kwa sababu umelipwa fedha; au ukiacha kuandika ukweli kwa sababu hiyo hiyo ya kulipwa fedha au ya kutishiwa, nayo ni makosa.
Sumaye alisema kufanya hivyo, kunavifanya vyombo vya habari vidharauliwe na hata kushitakiwa na kutakiwa kulipa fidia kubwa kwa kuvunja heshima ya watu au mtu. “Siyo sifa gazeti lako kuonekana linaandika habari za uwongo kila mara au dhahiri linatumika na kikundi fulani ili kuchafua kikundi kingine, labda kwa mashindano ya kibiashara au kisisasa, kama ambavyo tunashuhudia wakati wa chaguzi mbalimbali,” alisema Sumaye.
Aidha, akizungumzia juu ya kuzuia matangazo ya Bunge kuoneshwa moja kwa moja, Sumaye alisema kufanya hivyo ni kuvunja Katiba Ibara ya 18 (d) kuwa kila mtu ana haki ya kupewa taarifa wakati wote na kuzuia matangazo hayo hakuendani na mfumo wa demokrasia.
No comments:
Post a Comment