BIASHARA;Kiwanda cha General Tyre na reli hadi Arusha Kufufuliwa na serikali ya awamu ya tano.....................
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, amesema serikali ipo mbioni kufufua Kiwanda cha General Tyre, kufufua reli kutoka Arusha-Kilimanjaro pamoja na kiwanda cha Magadi ili kukuza uchumi na kuinua ajira kwa vijana. Hayo yalisemwa na Ntibenda wakati alipowahutubia wafanyakazi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kimkoa yaliyofanyika jana Viwanja vya Shehe Amri Abeid jijini Arusha. Aliwasihi wafanyakazi kutumia vyema vyama vya wafanyakazi mahali pa kazi ili walete maendeleo kati ya waajiri pamoja na wafanyakazi wenyewe. Alisema ni vyema wafanyakazi wakatumia vyama vyao vya wafanyakazi mahali pa kazi ili kuzungumza mambo yao mbalimbali na kusuluhisha, badala ya waajiri kuwazuia ili kuleta maendeleo. Alitoa rai kwa waajiri kuacha tabia ya kutowapa mikataba ya ajira wafanyakazi wao, badala yake washirikiane kwa pamoja katika kuleta maendeleo, kwani kampuni ikipata maendeleo wanaostahili pongezi ni wafanyakazi mnaoshirikiana nao kwa pamoja. “Fanyeni kazi na mtumieni vyama vya wafanyakazi katika kaleta maendeleo badala ya kuvitumia vyama vya wafanyakazi katika kuleta maendeleo nanyi waajiri acheni tabia ya kuwazuia wafanyakazi katika kuleta maendeleo badala ya kuwakandamiza,” alisema Ntibenda. Pia alisema serikali ipo mbioni kufufua viwanda pamoja na reli ili kuinua sekta ya viwanda pamoja kuinua uchumi kwa mkoa wa Arusha na kusisitiza vijana kufanya kazi badala ya kukimbilia kucheza ‘pool table’ pamoja na kupiga debe kwa kuwanyang’anya wananchi vitu vyao. Cosmas Chikoti ambaye ni Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi mkoa wa Arusha, aliomba serikali iangalie maslahi bora kwa wafanyakazi ikiwemo mikataba ya ajira pamoja na kusisitiza kuwa na mahusiano mema kati ya waajiri na waajiriwa. Hafla hiyo ilienda sambamba na maandamano ya wafanyakazi pamoja na kutoa zawadi kwa wafanyakazi bora ambapo pia wananchi mbalimbali walihudhuria ikiwemo wakuu wa wilaya za Arusha, wakurugenzi watendaji wa halmashauri na makatibu tawala mkoa na wilaya.
No comments:
Post a Comment