Monday, 2 May 2016

MICHEZO:Timu ya Pepsi ya jijini Arusha yapata kocha mpya..............




TIMU ya soka ya Pepsi ya jijini Arusha imeboresha kikosi chake kwa kumnyakua Kocha Jumanne Chale kukinoa kikosi hicho kinachojiandaa na ligi ya mabingwa ya mikoa katikati ya mwezi huu mkoani Singida.
Pepsi ilinyakua ubingwa wa ligi soka mkoa wa Arusha mwezi uliopita ikiwa chini ya kocha David Nyembele ambaye sasa amekuwa Mkurugenzi Mkuu wa ufundi wa bechi la timu hiyo.
Akithibitisha ujio wa kocha huyo, Nyembele alisema ni kutokana na kujiandaa vyema na ligi hiyo ili waweze kufanya vyema katika kituo cha Singida walichopangiwa.
Nyembele alisema Chale amewahi kufundisha timu mbalimbali za Ligi Kuu hapa nchini ikiwemo Ndanda na Prisons Mbeya na timu ya daraja la pili ya Kahama na timu kadhaa za jeshi na ana uwezo mkubwa wa ufundishaji.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa ujio wa kocha Chale kuifundisha timu ya Pepsi ni mafanikio makubwa kwao kwani ni kocha mkongwe na mzoefu wa ligi za hapa nchini hivyo wana uhakika wa kufanya vyema katika kituo cha Singida.
Alisema Pepsi tayari imeanza mazoezi katika viwanja vya shule ya sekondari ya Ilboru nje kidogo ya Jiji la Arusha na inafanya mazoezi ya asubuhi na jioni lengo ni kujiweka sawa na ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Mei 14 mwaka huu.
“Tumefanikiwa kumchukua kocha Chale lengo ni kuboresha bechi la ufundi ili timu iweze kufanya vyema katika kituo cha Singida na hatimaye kupanda daraja,’’ alisema.
“Tumejiandaa kupanda daraja na sio kushiriki ligi ya mabingwa kwani uongozi wa timu ya Pepsi una malengo makubwa na timu hiyo, ‘’alisema Mkurugenzi Nyembele.
Hata hivyo huenda ligi hiyo mabingwa wa mikoa ikasogezwa mbele kwani mpaka sasa timu za mikoa minane bado hazijakamilisha kuwasilisha mabingwa wa mikoa yao.
Mikoa ambayo bado haijapeleka mabingwa wao ni Njombe, Rukwa, Mbeya, Katavi, Kigoma, Tabora, Mara na wenyeji kituo cha Singida.
Pamoja na mikoa mingine kupeleka majina ya mabingwa wa Mikoa kwa Shirikisho la Soka nchini {TFF} lakini ni mikoa mitano tu imekamilisha kila kitu ikiwemo kulipa ada ya ushiriki wa ligi hiyo.
Mikoa hiyo ni Muheza Ltd ya Tanga, Makumbusho ya Kinondoni, Fire Stone ya Manyara, Stand Fc ya Pwani na timu ya Murusagamba Fc ya Kagera.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka TFF kuanza kwa ligi hiyo mwezi huu na tarehe iliyopangwa itakuwa ngumu sana kutokana na kasoro hizo za ulipati ada na zingine hazijakamilisha kabisa kupeleka majina ya wachezaji pamoja na kukiri kushiriki ligi hiyo.

No comments:

Post a Comment