Friday, 15 July 2016

CHUGA ROAD:Waliolipwa fidia kupisha ujenzi wa barabara Arusha watakiwa kuondoka

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga amewataka wakazi wa Arusha ambao wameshalipwa fidia kupisha ujenzi wa barabara ya Arusha Bypass kwa kubomoa nyumba zao haraka ili ujenzi wa barabara hiyo uanze mara moja.

Akizungumza mara baada ya kukagua barabara hiyo ya Arusha Bypass inayoanzia TPRI – Ngaramtoni –Oljoro hadi USA River yenye urefu wa km 42.4 Eng. Nyamhanga amewataka wakazi wanaopitiwa na ujenzi wa barabara hiyo kupisha eneo la ujenzi ili kumwezesha Mkandarasi kuanza kazi.

“Ni vema wananchi ambao mmeshalipwa fidia mkabomoa nyumba zenu wenyewe ili kupisha eneo la ujenzi kwani tayari kiasi cha shilingi bilioni 21 kimetolewa na Serikali kwa ajili ya fidia ili kuharakisha ujenzi wa barabara hii”, amesema Eng. Nyamhanga.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, (Sekta ya Ujenzi) amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya Sakina – Tengeru km 14.2 kuongeza kasi ya ujenzi ili kumaliza ujenzi huo ndani ya mkataba.

“Hakikisheni ujenzi wa barabara ya Arusha Bypass unaenda sambamba na kukamilika kwa barabara ya Sakina – Tengeru ili kuondoa msongamano katika barabara kuu ya Arusha – Moshi”, amesisitiza Eng. Nyamhanga.

Barabara ya Arusha Bypass km 42.4 na Sakina Tengeru km 14.2 ni sehemu ya barabara kuu ya Arusha – Moshi – Holili – Taveta hadi Voi yenye nia ya kupunguza msongamano katika ukanda wa Kaskazini inajengwa na kampuni ya Hanil na Jangsu toka Korea Kusini na China.

Barabara hiyo ya Arusha Bypass na Sakina – Tengeru zitakapokamilika zinatarajiwa kuwa na madaraja makubwa 7 na Makalvati 26 ambapo zaidi ya shilingi bilioni 164.4 zimetolewa na Benki ya Maendeleo Afrika na Serikali ya Tanzania kugharamia ujenzi huo.

Kukamilika kwa barabara hiyo licha ya kupunguza msongamano katika mji wa Arusha na Moshi pia kutakuza sekta ya utalii katika ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania.
Mkandarasi anayejenga barabara ya Arusha Bypass km 42.4 akitoa maelezo ya ujenzi huo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga alipokagua ujenzi wa barabara hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga wa pili kushoto akihakiki mchoro wa barabara ya Arusha Bypass inayoanzia eneo la TPRI Ngaramtoni hadi USA River km 42.4.
Muonekano wa barabara ya Arusha Bypass yenye urefu wa km 42.4 katika eneo la Ngaramtoni ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami inatarajiwa kupunguza msongamano katikati ya jiji la Arusha itakapokamilika. 
Wakazi wa eneo la Njiro jijini Arusha ambao wameshalipwa fidia kupisha ujenzi wa barabara ya Arusha Bypass wakiendelea kubomoa nyumba zao kabla ya kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga akijadiliana jambo na mkandarasi anayejenga barabara ya Arusha Bypass km 42.4 katika eneo la Oljoro alipokagua barabara hiyo.
Muonekano wa Bonde la Njiro litakapojengwa daraja kubwa katika barabara ya Arusha Bypass.

No comments:

Post a Comment