Monday, 26 September 2016

MKOANI MWANZA:Watanzania wang’ara Rock City Marathon 2016,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza awa kivutio, akimbia km 5

Chacha Masinde kutoka mkoani Mara akimaliza Rock City Marathon na kuwa mshindi wa kwanza kwenye mbio hizo zilizofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana . Chacha alitumia muda wa saa 01:03:00 kumaliza mbio hizo akifuatiwa na mshiriki kutoka nchini Kenya David Kilimo aliyetumia muda wa saa 01:04:40.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Bw John Mongella sambamba na maofisa kutoka benki ya NMB wakishiriki mbio  za  za km 5.
Washiriki wa mbio za km 21 wakiondoka Uwanja wa CCM Kirumba kuanza safari ndefu.
Ushindani ulikuwa ni mkubwa!
Washiriki kutoka pande tofauti za Dunia washiriki.
Ilikuwa ni furaha tupu kwa washiriki
Watoto nao hawakuwa nyuma…mbio zilihusisha watu kutoka rika zote kwa kuzingatia vigezo na mashariti.
Suala la usalama kwa washiriki ilikuwa miongoni mwa agenda za msingi kwenye mbio hizo.
Watu wenye ulemavu wa ngozi walishiriki mbio za km 5.


Mwandishi wetu, Mwanza



Chacha Masinde kutoka mkoani Mara ameibuka mshindi wa kwanza kwenye mbio za Rock City Marathon zilizofanyika jana jijini Mwanza baada ya kumaliza kwa muda wa saa 01:03:00, akifuatiwa na mshiriki kutoka nchini Kenya David Kilimo aliyetumia muda wa saa 01:04:40



Mbio hizo za kilomita 21 zilianzia Uwanja wa CCM Kirumba kupitia Barabara ya ikulu ndogo hadi mzunguko wa samaki na kuelekea Buzuruga kisha kutokea barabara ya pasiansi na kumalizikia uwanjani Kirumba huku Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella akishiriki kukimbia mbio za km 5 sambamba na watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino.



Nafasi ya tatu upande wa wanaume ilichukuliwa na Mkenya Moris Mosima aliyetumia muda wa saa 01:04:57, ikiwa sekunde chache nyuma ya mpinzani wake.



Akizungumzia siri ya ushindi wake, Chacha siri ya mafanikio hayo ni kujituma kwake zaidi katika kufanya mazoezi maalum kwa ajili ya mashindano hayo ili kuhakikisha kwamba mwaka huu mshindi wa kwanza katika mbio hizo anatoka nchini Tanzania tofauti na miaka ya nyuma ambapo washindi walikuwa wakitoka nchini Kenya.



 “Niliweka nadhiri nikasema mwaka huu lazima mshindi atoke Tanzania zaidi niwe mimi na ninashukuru nimetimiza adhama yangu. Pamoja na hilo maandalizi ya mwaka huu yamekuwa mazuri zaidi mahitaji yote muhimu yakiwemo maji tukiwa njiani yamesaidia mafanakinio hayo licha ya washiriki kuwa zaidi mwaka huu hatua ambayo iliongeza changamoto kwetu zaidi,’’ alisema.



Upande wa wanawake mshindi wa kwanza ni Mtanzania pia Faimina Abdi kutoka mkoani Arusha aliyetumia muda wa saa 01:13:12 akifuatiwa na mwenzake  kutoka mkoani Arusha Angelina Daniel aliyetumia saa 01:14:38 huku Mkenya Dorifine Omary akishika nafasi ya tatu akitumia saa 01:16:54



Washindi wa kwanza katika mbio hizo zilizofanyika kwa mara ya nane jijini Mwanza  waliibuka na kitita cha Sh1.5 milioni kila mmoja, washindi wa pili Sh900,000 na washindi watatu Sh700,000.



Mashindano hayo ya kila mwaka yaliyokatika kalenda ya RT yaliandaliwa na Kampuni ya Capital Plus kwa udhamini kampuni za Freidkin Conservation Fund na African Wildlife Trust, Benki ya NMB,  New Mwanza Hotel, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Real PR Solutions, kampuni ya Fabec, Tiper, Puma Energies, Clouds Fm, Jembe Fm, Barmedas Tv na EF Out Door.



Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi kwa washindi kwa washindi na washiriki wa wa mbio hizo Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Bw John Mongella ambae pia alishiriki mbio hizo kwa kukimbia mbio za km 5 alisema mbio hizo ni nyenzo muhimu ya kuwaandaa wanariadha nchini kuwa katika nafasi ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa na kuirudishia nchi heshima yake katika mchezo huo.



“Ndio maana tumekuwa tukisisitiza wadhamini waendelee kujitokeza kusaidia mbio hizi ili ziendelee kuwa bora zaidi,’’ aliongeza.



Akikabidhi zawadi kwa washindi wa mbio hizo kwenye uwanja wa CCM Kirumba kwa niaba ya Katibu tawala jana, Afisa michezo mkoa waMwanza James William alisema mbio hizo ni nyenzo muhimu ya kuwaandaa wanariadha wetu nchini kuwa katika nafasi ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa na kuirudishia nchi yetu heshima ya kipekee katika mchezo huo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.



Alisema: “Tanzania inaweza kurejea katika ramani ya dunia kwenye michezo kama tukijikita katika maandalizi mazuri ya kuibua na kuviendeleza vipaji vya vijana wetu nchini hasa kuanzia ngazi ya shule za msingi.”



Naye Mbunge wa jimbo la Ilemema ambae pia ni Naibu Waziri Wizara ya Ardhi, Ntumba na Maendeleo ya Makazi Bi Angelina Mabula alipongeza waandaaji wambio hizo na kutoa wito kwa washiriki walioshindwa kufanya vizuri kwenye mbio hizo kutokata tama bali wajiandae na mashindano yajayo ili waweze kufanya vizuri.


Naye Makamu Mwenyekiti wa mbio hizo Bw Zenno Ngowi alisema mbio hizo zimeweza kufanyika kwa mafaniko makubwa na ushirikiano walioupata kutoka uongozi wa mkoa wa Mwanza na mikoa jirani huku pongezi pia zikielekezwa  kwa jeshi la polisi kwa kuhakikisha kila kitu kinaisha kwa usalama

MKOANI MANYARA:Bodaboda Mirerani watakiwa kujipanga kulipia leseni ya usafirishaji

sim1
Mkuu wa Kituo cha polisi Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ASP Evarest Makala akizungumza juzi na wamiliki na madereva wa pikipiki katika warsha iliyoandaliwa na mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).
sim2
Mmiliki wa pikipiki Abubakary Sadiq akizungumza juzi mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Mnayara kwenye warsha iliyoandaliwa na mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).
sim3
Wamiliki na madereva wa pikipiki za kubeba abiria (bodaboda) wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani manyara, wakiwa katika warsha iliyoandaliwa juzi na mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).
……………………………………………………………
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mhandisi Zephania Chaula amewataka wamiliki na madereva wa pikipiki za kubebea abiria (bodaboda) kujiandaa kulipia mapato kupitia leseni ya usafirishaji wa abiria.
 
Mhandisi Chaula aliyasema hayo mji mdogo wa Mirerani, akizungumza na wamiliki na madereva wa pikipiki za kubebea abiria (bodaboda) kwenye semina iliyoandaliwa na mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).
 
Alisema wanapaswa kujiandaa na ulipaji wa leseni ya usafirishaji itakayoanza kutozwa hivi karibuni kwani haikwepeki, hivyo wajipange kwa ajili hiyo ili wachangie mapato ya nchi, ambayo inalenga kujitegemea.
 
“Hivi karibuni tutawapa taarifa ya kuanza kwa zoezi hilo ila sasa subirini kidogo kwani hii ni serikali ya awamu ya tano inayotaka kujitegemea kupitia mapato ya wananchi na siyo kuomba misaada nje ya nchi,” alisema Mhandisi Chaula.
 
Afisa mfawidhi wa Sumatra mkoani Manyara, Nelson Mmari alisema lengo la kukutana na bodaboda hao ni kuhakikisha kila mmiliki anakuwa na leseni ya usafirishaji inayotolewa kupitia halmashauri ya wilaya husika.
 
Mmari alisema Machi 2009, Bunge lilipitisha sheria ya kuruhusu pikipiki za magurudumu mawili au mitatu kubeba abiria kwa malipo au kukodisha na iliyoanza kutumika mwaka 2010 hivyo leseni ya usafirishaji inapaswa kulipiwa.
 
Alisema kila mtu anapaswa awe na leseni ya usafirishaji wa biashara ya kubeba abiria wa pikipiki ya magurudumu mawili au matatu na  atakayekiuka atatozwa faini ya kati ya sh50,000 au sh100,000 au kufungwa jela miezi sita au mwaka.
 
Alisema mkuu wa wilaya ya Simanjiro aliwaelewesha vizuri wamiliki na madereva wa bodaboda kuwa wajiandae na zoezi la ulipaji wa leseni ya usafirishaji kwani zoezi hilo linatarajia kuanza hivi karibuni kwenye eneo hilo.
 
Kwa upande wake, mkuu wa askari polisi wa usalama barabarani wa mkoa wa Manyara, Mary Kipesha, alisema wanasubiri taarifa ya mkuu wa wilaya hiyo ili waanze zoezi la ufuatiliaji ulipaji wa leseni ya usafirishaji kwa bodaboda.
 
“Tunasubiri mazungumzo hayo ila mjiandae na ninyi kwani baada ya hapo ndipo tutaanza ukamataji kwa wale ambao watakuwa hawajalipa leseni ya biashara ya kubeba abiria kwa wenye bodaboda hapa Mirerani,” alisema Kipesha